25 Mei 2025 - 23:09
Source: Parstoday
Muqawama walaani matamshi ya mbunge wa US anayetaka Gaza ipigwe mabomu ya nyuklia

Makundi ya Muqawama ya Palestina ya Hamas na Jihadul Islami yamemlaani vikali mbunge wa chama cha Republican nchini Marekani, Randy Fine kutokana na matamshi yake ya kutaka kufanyika shambulio la nyuklia katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na kurushwa na shirika la habari la Shehab la Palestina, Hamas imesema kuwa wito wa Fine wa kudondosha mabomu ya nyuklia huko Gaza unachochea mauaji ya halaiki na ni uhalifu wa wazi dhidi ya ubinadamu.

Harakati hiyo ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina imeeleza kwamba, matamshi hayo yanaakisi kile ilichokiita ubaguzi wa rangi wa kifashisti uliokithiri miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa Marekani, ambao unapaswa kulaaniwa na utawala wa Marekani na Congress.

"Wito wa matumizi ya silaha za maangamizi makubwa dhidi ya raia zaidi ya milioni mbili ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu na Mikataba ya Geneva," Hamas imeendelea kusema, ikisisitiza kwamba matamshi kama hayo hayatadhoofisha azimio la Wapalestina la kutetea haki zao halali, lakini badala yake yatafichua sura halisi ya utawala ghasibu wa Israel na wafuasi wake.

Msimamo huo wa Hamas umeungwa mkono na Harakati ya Jihadul Islami, ambayo pia ilitoa taarifa siku ya Jumamosi kujibu pendekezo hilo la kiwendawazimu la Fine.

Jihadul Islami imeyataja maoni hayo kuwa ya kibaguzi na yameegemezwa kwenye chuki, ambayo ni sawa na wito wa mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.

Mbunge huyo wa jimbo la Florida wa chama cha Republican, Randy Fine katika mahojiano na Fix News aliashiria shambulio la bomu la atomiki la Marekani dhidi ya Wajapan huko Hiroshima wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na kutoa wito wa kuangamizwa Gaza kwa silaha za nyuklia.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha